29 Septemba 2021 - 14:37
Takht Ravanchi: Baraza la Usalama linapasa kuilazimisha Israel ihitimishe uvamizi wake Syria

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amelitaka Baraza la Usalama la umoja huo kuilazimisha Israel ili isitishe mara moja uvamizi na chokochoko zake dhidi ya mamlaka na umoja wa ardhi nzima ya Syria.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Majid Takht Ravanchi ameeleza hayo jana katika kikao cha Baraza la Usalama kuhusu matukio ya kisiasa na kiusalama ya Syria. Ravanchi amesisitiza kuwa chokochoko za Israel dhidi ya mamlaka ya kujitawala na ya umoja wa ardhi nzima ya Syria zinakiuka sheria za kimataifa na kwamba hatua za kiuhasama za utawala wa Kizayuni zinatishia amani na usalama wa eneo na kimataifa. 

Katika kikao hicho, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametilia mkazo pia ulazima wa kuendelea mapamano dhidi ya makundi ya kigaidi huko Syria na kueleza kuwa vita dhidi ya makundi ya kigaidi havipasi kusitishwa kwa sababu hatua za uharibifu za makundi hayo ni tishio kwa usalama na umoja wa ardhi nzima ya Syria na pia kwa amani na usalama wa eneo.

Mwishoni mwa hotuba yake, Majid Takht Ravanchi amesisitiza kuwa, vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Syria vinapasa kuondolewa na kukariri uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi na serikali ya Syria ili kurejesha umoja na mshikamano wa ardhi yote ya nchi hiyo. 

342/